Mada ndogo: Insha za kubuni
3.3.1 Maana ya insha
Insha ni maandishi yanayowasilisha mawazo, maelezo, hoja au matukio kuhusu mada fulani.
Insha huandikwa kwa kufuata mpangilio unaowezesha msomaji kuelewa ujumbe.
3.3.2 Maana ya insha ya kubuni
Insha ya kubuni ni insha ambayo mwandishi hutumia mawazo na ubunifu wake kuunda kisa au kueleza jambo fulani.
Insha hii inaweza kuwa na matukio ya kufikirika au matukio yaliyobuniwa kutokana na maisha ya kawaida.
3.3.3 Hatua za kuandika insha ya kubuni
Hatua ya kwanza: Kuchagua mada
Mwandishi anapaswa kuchagua mada anayoielewa na anayeweza kuandika kuihusu.
Mifano:
Siku ambayo sitaisahau.
Safari ya kwenda mjini.
Rafiki yangu mpya.
Tukio la kushangaza shuleni.
Umuhimu wa kusaidiana.
Hatua ya pili: Kutambua ujumbe
Mwandishi anapaswa kuamua jambo kuu analotaka kuwasilisha.
Mfano:
Mada: Siku ambayo sitaisahau.
Ujumbe: Umuhimu wa kusaidia wengine wakati wa matatizo.
Hatua ya tatu: Kuandaa vidokezo
Vidokezo ni mawazo muhimu yanayomsaidia mwandishi kupanga insha.
Mfano wa vidokezo:
Kuamka asubuhi.
Kujiandaa kwenda shuleni.
Kukutana na mtoto aliyekuwa akilia.
Kumsaidia mtoto huyo.
Kumfikisha nyumbani.
Kushukuruwa na wazazi wake.
Hatua ya nne: Kupanga vidokezo
Vidokezo vinapaswa kupangwa kulingana na mtiririko wa matukio.
Hatua ya tano: Kuandika insha
Mwandishi hutumia vidokezo kuandika aya zinazoeleweka.
Hatua ya sita: Kuhakiki insha
Insha inapaswa kusomwa tena ili kurekebisha makosa ya:
Sarufi.
Tahajia.
Viakifishi.
Mpangilio wa mawazo.
Matumizi ya msamiati.
3.3.4 Muundo wa insha
Insha nzuri huwa na sehemu tatu kuu.
1. Utangulizi
Hii ni sehemu ya mwanzo inayomtambulisha msomaji kuhusu mada au kisa.
Utangulizi unapaswa kuvutia msomaji.
2. Mwili wa insha
Hii ndiyo sehemu kuu inayotoa maelezo, hoja au matukio.
Mawazo yanapaswa kupangwa katika aya zinazofuatana kimantiki.
3. Hitimisho
Hii ni sehemu ya mwisho inayofunga insha.
Inaweza kutoa funzo, matokeo ya tukio au ujumbe wa mwandishi.
3.3.5 Sifa za insha nzuri ya kubuni
Huwa na kichwa kinachofaa.
Huwa na ujumbe unaoeleweka.
Huwa na utangulizi mzuri.
Mawazo hupangwa kwa utaratibu.
Hutumia msamiati unaofaa.
Hutumia viakifishi ipasavyo.
Huwa na aya zilizounganishwa vizuri.
Huwa na hitimisho linalofaa.
Huonyesha ubunifu wa mwandishi.
3.3.6 Mfano wa mpangilio wa insha
Mada: Siku ambayo sitaisahau
Vidokezo:
Kuamka asubuhi.
Kujiandaa kwenda shuleni.
Kukutana na tukio lisilotarajiwa.
Kuwasaidia watu waliokuwa na matatizo.
Kupata shukrani.
Kujifunza umuhimu wa ukarimu.